Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kampuni ya Kijerumani ya Bosch imeamua kufunga ofisi yake ya Akili Mnemba nchini Israel, hatua hii ni tukio la kwanza la kufungwa kwa kituo cha nje cha kampuni hiyo tangu janga la COVID-19. Vilevile, Bosch ndiyo kampuni kubwa ya kwanza ya Kijerumani kuondoka katika mfumo wa utafiti wa Israel.
Msemaji wa kampuni hiyo alithibitisha kwamba uamuzi wa kufunga ofisi hiyo ulifanyika mwezi Desemba, na wafanyakazi walijulishwa kuhusu jambo hilo mwezi Januari, alisisitiza kwamba uamuzi huu umechukuliwa kwa sababu za kiuchumi.
Bosch ilikuwa imeanza shughuli zake za utafiti nchini Israel tangu mwaka 2018, kampuni hii ilikuwa ikifanya kazi kupitia “Kituo cha Akili Bandia cha Bosch” katika miji ya Tel Aviv na Haifa.
Ofisi zinazofanya kazi katika sekta za akili bandia, vihisishi (sensors), na mifumo ya otomatiki ziko katika mchakato wa kufungwa, na inatarajiwa kwamba mchakato huo utakamilika mwishoni mwa mwezi Juni.
Hata hivyo, Bosch itaendelea na uwepo wake wa kibiashara nchini Israel kupitia kampuni zake tanzu zikiwemo BSH, Elmo Motion Control na Bosch Ventures.
Mazingira ya vita yameyumbisha uthabiti wa shughuli za uendeshaji
Andrea Fram, mkuu wa ofisi ya Tel Aviv ya Umoja wa Vituo vya Utafiti vya Ujerumani (Helmholtz), katika kauli zake alizungumzia athari za vita kwa shughuli za kampuni za kigeni nchini Israel.
Alisema kuwa; tangu tarehe 7 Oktoba 2023 hadi sasa, wataalamu wa Kijerumani hawajaonesha hamasa kubwa ya kwenda kuishi na kufanya kazi nchini Israel, na familia zenye watoto pia zimechukua mtazamo kama huo.
Kwa mujibu wa Fram, mazingira ya kivita yaliyotawala eneo hilo yameathiri kwa kiasi kikubwa uthabiti wa shughuli za uendeshaji.
Alisisitiza kwamba; kampuni za Kijerumani, bila kuwa na mtazamo ulio wazi na uhakika kuhusu hali za baadaye, hazitakuwa na nia ya kufungua ofisi mpya katika eneo hilo.
Wachambuzi pia wanaamini kwamba mfumo wa ubunifu wa Israel umefikia hatua nyeti na yenye kuamua mustakabali wake. Kwa mujibu wao, kufuatia migogoro ya kimataifa na kuendelea kwa vita, uwekezaji katika sekta ya teknolojia nchini Israel umeshuka hadi kiwango chake cha chini kabisa tangu mwaka 2018.
Maoni yako